Yuda akakwea; naye Bwana akawatia Wakanaani na Waperizi mkononi mwao; nao wakawapiga huko Bezeki watu elfu kumi.
Wakampata huyo Adoni-bezeki huko Bezeki; wakapigana naye, nao wakawapiga Wakanaani na Waperizi.
Lakini Adoni-bezeki akakimbia; nao wakamwandamia na kumshika, wakamkata vyanda vyake vya gumba vya mikono na vya miguu.
Adoni-bezeki akasema, Wafalme sabini, waliokuwa wamekatwa vyanda vyao vya gumba vya mikono na vya miguu, waliokota chakula chao chini ya meza yangu; kama nilivyofanya mimi, Mungu amenilipa vivyo. Wakamleta Yerusalemu naye akafa kuko.