Ndipo Yaeli, mkewe Heberi, akatwaa kigingi cha hema, akashika nyundo mkononi mwake, akamwendea polepole, akamtia kile kigingi katika kipaji chake, nacho kikapenya, hata kuingia mchangani; kwa maana usingizi mzito ulikuwa umemshika; basi akazimia, akafa.
Na tazama, Baraka alipokuwa akimfuatia Sisera; Yaeli akatoka ili kumlaki, akamwambia, Njoo, nami nitakuonyesha yule mtu unayemtafuta. Basi akamwendea, na tazama, Sisera amelala humo, amekufa, na hicho kigingi kilikuwa kipajini mwake.
Akanyosha mkono wake akashika kigingi, Nao mkono wake wa kuume ukashika nyundo ya fundi; Akampiga Sisera kwa hiyo nyundo, akamtoboa kichwa chake. Naam, alimpiga akamtoboa kipaji chake.