Haya, jichagulieni watu watatu kwa ajili ya kila kabila; nami nitawatuma, nao watainuka waende kati ya hiyo nchi, na kuiandika kama urithi wao ulivyo; kisha watanijilia mimi.
Basi watu hao wakainuka wakaenda; kisha Yoshua aliwaagiza wale waliokwenda kuiandika nchi, akawaambia, Endeni, mkapite katikati ya nchi, na kuiandika habari zake, kisha mnijie tena hapa, nami nitawapigia kura kwa ajili yenu hapo mbele za Bwana huko Shilo.